Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe. Simon Simalenga amewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaficha watoto kwa kuwanyima fursa ya kupata chanjo ya matone ya Polio awamu ya nne ambayo itaanza rasmi kutolewa kwa siku nne kuanzia Disemba Mosi, 2022 kwa watoto wote hata kama alipata chanjo hiyo awamu za awali.
Mkuu wa Wilaya, Mhe. Simon Simalenga ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Afya Msingi ya Wilaya ambayo imekutana kwa ajili ya kuweka mikakati ya kutoa chanjo hiyo kwa watoto wengi zaidi ya wale waliopata matone katika awamu ya kwanza, pili hata ya tatu, kikao ambacho kimefanyika Ukumbi wa Social uliopo Kata ya Mkwajuni.
Mhe. Simalenga amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wazazi kuwaficha watoto wakiwanyima nafasi ya kupata chanjo jambo ambalo linahatarisha afya na maisha ya watoto hao, akisema ugonjwa huo ni hatari kama hakutakuwa na kinga za mapema.
“Madhara ya hili gonjwa (Polio) jamani ni makubwa sana, tofauti na unavyoweza kufikiria, lazima tuhakikishe watoto chini ya miaka mitano wanapata chanjo hii”, alisema Mkuu wa Wilaya ya Songwe akizungumza kwenye kikao hicho.
Mhe. Simalenga ameongeza kuwa anahitaji kuona utolewaji wa chanjo ya Polio unaenda kwa kasi ili kufikia makadirio ambayo Wilaya ya Songwe imepangiwa kuwapatia matone watoto kwenye awamu hii ya nne.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songwe Egfrid Mwingiliela ameieleza kamati hiyo kuhakikisha kampeni ya nyumba kwa nyumba inakuwa shirikishi ili mzazi au mlezi kuhamasika kumtoa mtoto wake kupata matone ya chanjo ya Polio.
Wilaya ya Songwe inaingia katika utekelezaji wa awamu ya nne ya utolewaji wa chanjo ya matone ya polio kwa watoto waliochini ya miaka mitano kufuatia utekelezaji wa awamu ya kwanza, pili na hata ya tatu utekelezaji wake kufanikiwa kwa zaidi ya asilimia 100.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.