Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe. Solomon Itunda amemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe kuhakikisha anazishirikisha taasisi za serikali katika miradi mbalimbali inayotekelezwa wilayani hapa ili kupunguza changamoto ambazo zinaibuka kutokana na kutoshirikishwa kwa taasisi hizo kama Zimamoto, RUWASA, TANESCO na TARURA.
Mhe. Itunda ametoa maelekezo hayo baada ya ukaguzi wa mradi wa Kituo cha Afya Ifwekenya ambacho kitakaguliwa na kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru 2023 ambapo amesema taasisi zinaposhirikishwa zinaweza kushauri sawa na miongozo yao ili kupunguza kurudia rudia marekebisho ambayo yangefanyika tangu awali.
"Zimamoto wana taratibu zao zakiuokozi panapotokea janga la moto watashauri milango na madirisha yakae kwa mpangilio upi, watu wa maji nao wanajua namna bora ya kusogeza huduma ya maji ...na taasisi nyingine, shirikisheni Taasisi hizi za serikali hususan kwa miradi inayoendelea Wilayani Songwe kujengwa", alisema Mkuu wa Wilaya huyo.
Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo ameipongeza Halmashauri inayoongozwa na Mwenyekiti Mhe. Abrahamu Sambila Diwani wa Mbangala pamoja na CPA. Cecilia Kavishe kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Ifwekenya ambacho kukamilika kwake kitakuwa suluhu ya adha ya wananchi wa Kata hiyo.
Ndg. Abdallah Mgonja, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe amesema kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri baraza la madiwani limetenga fedha shilingi 60,000,000 kwa mwaka wa fedha 2023/24 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha Afya ambacho kinajengwa kwa mapato ya ndani kwa asilimia 100 ambapo mpaka sasa kimegharimu zaidi ya milioni 500.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.