Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe. Solomon Itunda amewataka viongozi wa vitongoji na vijiji pamoja na Divisheni ya mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe kuhakikisha wanasimamia mpango wa taifa wakupanda miti mitano kwa kaya za mjini na miti kumi kwa kaya za vijijini ukiwa ni mpango wa awali wa utunzaji wa mazingira.
Mhe. @solomonitunda amesema hayo wakati akiongea na wananchi wa kijiji cha Saza Wilayani Songwe katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2023 ambapo amesema upandaji wa miti kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo husika ukisimamiwa vizuri utasaidia kuvifanya vyanzo vya maji kudumu muda mrefu, na utasaidia mvua kuendelea kunyesha.
Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo amepiga marufuku ujenzi holela ambao umekuwa ukichochea uharibifu wa mazingira, uchimbwaji holela wa madini pamoja na kufanya shughuli za kilimo kwa uvunaji wa misitu holela.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe Mhe. Abrahamu Sambila akiongea katika maadhimisho hayo amewasihi wananchi wa Kata ya Saza na Wilaya ya Songwe kwa ujumla kuachana na ukataji miti hovyo ili mazingira yaendelee kuvutia mvua.
CPA. Cecilia Kavishe, Mkurugenzi Mtendaji wa Songwe DC akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Songwe wakati wa maadhimisho amesema wamechagua kuadhimisha katika kijiji cha Saza kutokana na shughuli za uchimbaji madini ambazo zimekuwa zinafanywa na wachimbaji wadogo na wakubwa shughuli ambazo zimekuwa zinahusisha ukataji wa miti na uchimbaji karibu na vyanzo vya maji.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 05 ambapo mwaka 2023 maadhimisho hayo yamebeba ujumbe wa "Pinga Uchafuzi wa Mazingira Unaotokana na Taka za Plastiki".
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.