Wakulima wa Kijiji cha Magamba, Kata ya Magamba Wilayani Songwe mkoa wa Songwe wameishukuru serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Songwe kwa kuanzisha mfumo wa uuzaji wa zao la ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao wameutaja kuwa mkombozi wa kilimo chao.
Wakulima hao kwa nyakati tofauti wamezungumza hayo baada ya kumalizika mnada wa tatu wa ufuta Wilayani Songwe huku bei zikiendelea kupaa katika kila mnada kuanzia uliofanyika Mei 5 hadi Jumatano Mei 24, 2023.
Bi. Pelegia Boniface Simfukwe, 38, akizungumza kando na ghala la Magamba ambako mnada umefanyika amesema amekuwa akilima ufuta kwa muda mrefu hajawahi kuuza ufuta wake katika bei inayokaribiana na mnada wa Leo [Jumatano Mei 24].
"Tulikuwa tunauza ufuta lakini hii bei ni nzuri kwetu wakulima, mwanzoni bei ilikuwa ikipanda sana inakuwa 2,500 hadi 3,000 lakini sasa tumeuza 3,678", alisema Bi. Pelegia akiwa amejifunga kilemba kichwani.
Christopher Yunji akizungumza baada ya mnada amesema anaipongeza serikali kwa kuleta mfumo wa stakabadhi ghala ingawa amekiri wazi kwamba mwanzoni alikuwa anahofia lakini sasa amepata uelewa wa namna unavyoendeshwa ataenda kuwahamasisha wakulima wengi zaidi.
Pongezi hizo zimetolewa pia na Willy Julius Msukwa ambaye pia ni mkulima wa kijiji cha Magamba ambaye amesema kutokana na mfumo huo anategemea uchumi wa familia yake kuimarika ambapo ameomba serikali kwa mwaka ujao kuanza masoko mapema zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe CPA. Cecilia Kavishe akizungumza kwenye mnada huo amewaeleza wananchi kuwa kutokana na mfumo wa stakabadhi ghalani Halmashauri inategemea kupata takwimu sahihi za wakulima lakini pia itaanza kugawa mbegu za ufuta bure kwa wakulima kuanzia msimu ujao wa kilimo pamoja na ili kuongeza kasi katika uzalishaji.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe Mhe. Godian Wangala alimwakilisha mwenyekiti wa Halmashauri amesisitiza suala la mkulima kuwa huru kuanza ufuta wake popote pale ndani ya Wilaya ya Songwe isipokuwa mnunuzi hataruhusiwa kuuza ufuta huo bila kupitia stakabadhi ghalani.
Kuhusu minada ya mara kwa mara, Mhe. Wangala amesema kama Halmashauri wanaendelea kuratibu kuona namna ya kuboresha tarehe ya mnada mmoja na unaofuata ili kumfanya mkulima auze zao lake kiurahisi na bei nzuri.
Mnada wa Leo Jumatano, ghala la Magamba ni wa tatu kwa Songwe DC katika mkoa wa Songwe ambapo takribani tani 1555.773 sawa na kilo 1,555,773 zimeuzwa kwa shilingi 3,678.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.