Wanawake Wilayani Songwe mkoani Songwe wameaswa kuwa wathubutu katika matumizi ya teknolojia kwenye shughuli wanazofanya ili kuendana na kasi ya dunia.
Mwito huo umetolewa na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Songwe Ndg. Godwin Kaunda ambaye ni Afisa Tarafa ya Songwe Jumanne Machi 08, wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo Kiwilaya yamefanyika Kata na kijiji cha Saza.
Ndg. Kaunda amesema ili wanawake wapate mafanikio makubwa ni lazima waweke kujifunza kwenye teknolojia ambayo itawawezesha kuanzisha miradi ya kisasa kama mashine, viwanda vidogo vidogo kupitia mikopo ya asilimia 10 ambayo hutolewa na Halmashauri mbalimbali nchini kupitia mapato ya ndani.
Kutokana na uwepo wa vikundi ambavyo vina mitaji midogo, Ndg. Kaunda amemsihi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe kuongeza ukopeshaji wa fedha kwa wanawake ili waweze kufungua viwanda vitakavyowasaidia kujiimarisha kiuchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla.
Kutokana na nasaha hizo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe Mhe. Godian Wangala ambaye ni Diwani wa Kata ya Totowe amesema kupitia vikao vyao watashauriana na wataalamu kuona namna mikopo ambayo inatolewa iongozwe kwenye vikundi ili viweze kufungua viwanda ambavyo vitaendana na wakati uliopo wa teknolojia kuliko kuendelea kutumia nyezo tata na teknolojia nyingine za zamani.
Pamoja na hayo, Mhe. Wangala amewapongeza wanawake ambao wanamikopo ya asilimia 10 katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe kwa kuwa vinara katika marejesho kulinganisha na makundi ya vijana na watu wenye mahitaji maalumu.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka Machi 08 ingawa hutanguliwa na maadhimisho kama hayo ngazi ya Wilaya lengo ni kutambua thamani ya mwanamke katika usawa wa kijinsia.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.