Wananchi wamehimizwa kuchangamkia fursa za usogezaji wa mawe, upondaji wa kokoto katika ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa eneo la Kikuyuni kupitia Mradi wa Boost.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe. Solomon Itunda akizungumza mara baada ya shughuli ya kuchimba msingi wa kuanza ujenzi wa shule hiyo kwa kushirikiana na wananchi wa kitongoji cha Kikuyuni Kata ya Mkwajuni uliyofanyika Mei 3, 2023.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe amesema Mradi wa Boost unatakiwa ku'boosti' hata maisha ya wananchi wa kawaida ili mbali na maboresho ya kielimu pia wananchi uchumi wao uwe bora.
Amesema ujenzi wa shule hiyo mpya yenye madarasa saba ya shule ya msingi na madarasa mawili kwa shule ya awali (mfano) wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa za kuponda kokoto, kusogeza mawe kwa ajili ya ujenzi wa msingi.
"Tunataka hizi hela zisitoke hapa kwetu [Songwe DC] sogezini mawe, pondeni kokoto mtapata hela na shule itajengwa ili watoto wenu wasome hapa", alisema Mhe. Itunda ambaye alikuwa ameambatana na viongozi mbalimbali ngazi ya Wilaya.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songwe Ndg. Mabrouck Mwaiswelo amewasihi wananchi wa kijiji cha Kaloleni kuendelea kumuombea afya njema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na kuendelea kuigusa Wilaya ya Songwe katika miradi mikubwa ya maendeleo, akisema pongezi za kutosha ni kumpa kura za kutosha kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
CPA. Cecilia Kavishe, Mkurugenzi Mtendaji Songwe DC amewaambia wananchi kuwa Mama Samia ameipatia Kikuyuni milioni 538 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule ya awali na msingi.
CPA. Cecilia Kavishe amewahimiza wanawake kujitokeza zaidi kuponda kokoto ili waimarishe uchumi wao na familia zao.
Mwakilishi wa wananchi Kata ya Mkwajuni Mhe. Shaibath Kapingu akizungumza kwenye shughuli hiyo ameipongeza serikali ya Rais Samia huku akiomba Tarura kuwasaidia kujenga barabara ili vifaa vifike kwenye eneo la mradi kiurahisi.
Halmashauri ya Songwe DC imepokea bilioni 1.04 kupitia Mradi wa Boost kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu awali na msingi, kijiji cha Kaloleni ndiyo iliyopokea fedha nyingi kulinganisha na maeneo Wilayani hapa.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.