Wakulima wa mazao mbalimbali wilayani Songwe mkoani Songwe wameaswa kujikita katika kilimo cha kisasa ambacho kinaelezwa kuwa na tija kubwa kwa mkulima mmoja na mmoja, taifa kijamii na kiuchumi na kijamii.
Kauli ya hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe. Simon Simalenga Leo Jumatano wakati akizungumza kwenye kikao cha wadau wa kilimo wilayani Songwe kama Meru Agro Tours and Consultant Ltd na kampuni nyingine kikiwa na malengo ya kuona namna ya kumwinua mkulima kwa kumpatia mbolea na pembejeo za kilimo kwa wakati na bei rafiki kilichofanyika katika ofisi za mkuu wa wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya Mhe. Simalenga amesema dhana ya kuwa Wilaya ya Songwe ina rutuba nzuri kiasi kwamba haipaswi kutumika mbolea na pembejeo nyingine za kisasa imepitwa na wakati hivyo wakulima ni muhimu kuanza kutumia mbolea na mbegu za kisasa ili kuongeza uzalishaji sawa na maeneo mengine kama Wilaya ya Mbozi.
Mhe. Simalenga amesema uwepo wa mbolea ya ruzuku ni nia ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuona wakulima wanainuka kiuchumi kwa kuongeza uzalishaji wa mazao mengi na bora ili kushindana sokoni na mataifa jirani.
Pia, Mhe. Simalenga amewataka wauzaji na mawakala wa mbolea na pembejeo ambao hawana ofisi makao makuu ya wilaya (Mkwajuni) kuanzisha ofisi eneo hilo ili kuwapunguzia gharama wakulima ya kusafiri umbali mrefu kufuata mbolea.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe Mhe. Wangala akichangia katika kikao hicho ameeleza umuhimu wa wakulima wakimemo wakulima wa korosho kupewa elimu ya namna ya kujihusisha na kilimo bora na cha kisasa, ambapo amesema baadhi ya wakulima hawana misingi ya kilimo cha kisasa.
Abdukadir Mfilinge, Afisa Kilimo na Umwagiliaji Wilaya ya Songwe amewahimiza wakulima ambao bado hawajajiandikisha kwenye mfumo wa kupata mbolea ya ruzuku kujiandikisha kwenye maeneo husika kwani lengo la serikali ni kuona kila mkulima ananufaika na punguzo hilo.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.