Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Songwe Ndg. Chesko Mbilinyi amewahimiza Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Waalimu Wakuu na Waalimu wa Takwimu kuandaa na kutoa taarifa sahihi kwenye mfumo ambazo zitaiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Songwe na taifa kwa ujumla kupanga mipango ya maendeleo.
Kaimu Katibu Tawala huyo ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo kwa washiriki hao yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Maweni iliyopo Mkwajuni Leo Alhamis Machi 22, ambapo amewasisitiza umuhimu wa kutoa taarifa sahihi ambazo hazijapikwa.
Ndg. Mbilinyi amesema kama kutakuwa na upikaji wa taarifa katika ngazi za chini kutakuwa na mipango ambayo haiendani na idadi ya wanafunzi, waalimu na miundombinu mingine.
"Tunataka taarifa sahihi, bila taarifa sahihi hatutaweza kupanga bajeti yenye uhalisia. Upanga wa bajeti nzuri inayoakisi mahitaji yetu inategemea taarifa ambazo zitaifikia Halmashauri na serikali Kuu" alisema Chesko Mbilinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mafunzo hayo.
Kaimu Afisa Elimu Sekondari Alumine Kaminyoge ameeleza kuwa mafunzo hayo kama kila mmoja atayatumia vizuri yatakuwa chachu kwenye jamii kwani kutakuwa na maendeleo sawa na mahitaji.
Anthony Jamula, Mwezeshaji wa mafunzo ambaye pia ni Afisa Elimu Vifaa na Takwimu, Idara ya Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ameeleza kuwa mafunzo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki ili kuanzia Aprili Mosi taarifa zianze kujazwa kwenye mfumo, akisisitiza kwamba siyo tu taarifa bali taarifa sahihi.
Mafunzo hayo ya siku moja yamelenga kuongeza hamasa ya uandaaji wa taarifa sahihi za shule [School Information System] na Sensa ya Elimu [Annual School Census].
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.