Mkoa wa Songwe umevuka lengo la ukusanyaji wa mapato katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Mhe. Waziri Waziri Kindamba, Mkuu wa Mkoa wa Songwe ametoa taarifa hiyo kwenye kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Halmashauri robo ya kwanza ya 2022/2023, kilichofanyika Ijumaa Novemba 11, 2022.
Mhe. Kindamba amesema kuwa alipoingia katika mkoa wa Songwe malengo yake makubwa yalikua ni mambo matatu ikiwemo ukusanyaji mapato, kusikiliza kero za wananchi na kuimarisha ulinzi na usalama.
‘’Napata faraja kubwa kuona katika suala la mapato kama mkoa tumevuka lengo katika robo ya mwaka huu ilikua ni kukusanya bilioni 6.5 lakini kwa kipindi hiki cha robo hii tumekusanya 8.6 bilioni’’ amesema Kindamba.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo unataka fedha ikiwa ni ujenzi wa madarasa, vituo vya afya, dawa katika vituo vya afya na maji.
Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unahitaji ukusanyaji wa mapato.
‘’Ukitaka kugombana na mimi zembea katika kukusanya mapato, ukiona nagombana na wewe ujue nasimamia misingi na maadili ya kazi yangu’’ alisisitiza Kindamba akiongea hayo mbele Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Mipango, Maendeleo ya Jamii, Wahazina na Maafisa Habari.
Pia, Kindamba ameshauri kuwa katika Halmashauri ambazo hazijafanya vizuri waende ofisi ya katibu tawala mkoa akawashauri ni njia zipi zitaweza kuwanasua sehemu waliopo kwa sasa ili waweze kufanya vizuri kama Halmashauri zingine.
‘’Mimi ni mwalimu na lengo langu ni kutekeleza wajibu na huwa walimu tukiona watu wetu wanafanya vizuri tunafurahi mje ofisini kama kuna changamoto yoyote tupeane ushauri wapi kuna changamoto’’ amesema
Amebainisha kuwa lengo la mkoa ni kila Halmashauri kukusanya mapato zaidi ya asilimia mia.
Hata hivyo ameshauri kuwa kwa Halmashauri zinazofanya vizuri ziangalie vyanzo vinavyofanya vizuri juhudi ziongezwe katika kudhibiti mapato kuepuka mianya ya utoroshwaji wa mapato.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa Halmashauri zinatakiwa kubuni vyanzo vya mapato kupitia fursa zilizopo katika mkoa huo.
"Bunge limesisitiza asilimia 10 zinazotengwa na Halmashauri kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu mhakikishe mnazisimamia" aliongeza.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.