Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe. Simon Simalenga amesema Tanganyika imeyafikia maendeleo makubwa katika miaka 61 ya Uhuru akiwataka watanzania kujivunia maendeleo hayo.
Mhe. Simalenga amesema hayo wakati akifungua kongamano la kujadili maendeleo ambayo Wilaya ya Songwe imeyafikia tangia taifa la Tanganyika kuwa huru mnamo 09.12.1961.
Ametaja amani, mshikamano, na upendo uliopo, masuala ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao kulinganisha na miaka hiyo akisema haya ni maendeleo ambayo Tanzania Bara imeyapata kwa sababu kama taifa ni wamoja na wenye upendo, akisema mataifa ambayo hayana amani ni vigumu kupata maendeleo kwenye nyaja za kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Simalenga amesisitiza juu ya wakulima na wafugaji kulima na kufuga kisasa akisema katika miaka 61 ya Uhuru hakuna haja ya mfugaji kuendelea kufunga kimazoea, bila tija, wala mkulima kulima kilimo cha asili wakati mbinu bora zipo kama kutumia mbolea na pembejeo nyingine za kilimo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe CPA. Cecilia Kavishe akizungumza katika kongamano hilo amewaeleza wajumbe na wananchi juu ya maendeleo mbalimbali yaliyofikiwa kwa wakati huu ambayo hayakuwepo nyakati Tanzania Bara inapata Uhuru wake mwaka 1961.
Mkurugenzi Mtendaji CPA. Cecilia Kavishe ameeleza kuwa miradi mingi ambayo sasa wanasongwe wanajivunia kama Ujenzi wa Vituo vya Afya, Zahanati, Shule ya Sekondari na Msingi ambazo zinajengwa ikiwemo madarasa ya Uviko, pamoja na utolewaji wa huduma bora kwa wananchi ni sehemu ya mambo ambayo serikali kupitia awamu mbalimbali za uongozi imezifanya kwa manufaa ya watanzania wenyewe.
Naye Abdukadir Mfilinge, Afisa Kilimo na Umwagiliaji akieleza mafanikio ambayo Wilaya imeyapata kwenye kilimo amesema taifa limepiga hatua kubwa mathalani Wilaya ya Songwe inategemea kilimo kama chanzo cha mapato ambapo ukiondoa madini, mazao ya kilimo ni chanzo cha pili kwenye ukusanyaji wa mapato.
Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo Musa Twalib ameomba miradi yote ya maendeleo iwe shirikikishi ili jamii ijione ni sehemu ya huo mradi suala ambalo litasaidia hata katika kuulinda.
Kongamano la miaka 61 ya Uhuru 2022 lilikuwa na Kauli Mbiu ya "Amani na Umoja ni Nguzo ya Maendeleo Yetu" ambapo kwa mwaka huu maadhimisho yake yamefanyika kwa kila Wilaya kuandaa sherehe zake.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.