Kamati Simamizi ya Mradi wa Boost ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Songwe imetambulisha Mradi wa Boost ambao unaenda kuboresha na kujenga miundombinu ya elimu katika Divisheni ya Elimu Awali na Elimu Msingi kwa shule mbalimbali.
Mratibu wa Mradi Wilaya ya Songwe Ndg. Lucian Yunga akizungumza na Viongozi wa Kata ya Mkwajuni wakati wa kutambulisha Mradi huo shughuli iliyofanyika Shule ya Msingi Mkwajuni Jumanne Aprili 11, 2023 amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga zaidi ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa kata ya Mkwajuni pekee.
Yunga ameeleza kuwa kati ya fedha hizo, milioni 538,500,000 ni ajili ya ujenzi wa vyumba saba vya Shule ya Msingi Kikuyuni, vyumba vya madarasa viwili vya awali [Shule ya Mfano] pamoja na matundu sita ya vyoo.
Wakati huo milioni 50,000,000 zinaenda kujenga miundombinu ya vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Osterbay ambayo pia matundu matatu ya vyoo yatajengwa kwa milioni sita.
Katika hatua nyingine, Yunga amewahimiza viongozi wa vijiji kutenga maeneo ambayo ni salama kwa wanafunzi kufika shuleni lakini maeneo ambayo hayana migogoro ya wananchi kwa wananchi ama wananchi na serikali.
Mhasibu wa Mradi wa Boost ngazi ya Halmashauri, Noel Hango amewaomba viongozi wa Kata na vijiji kusimamia kwa uzalendo miradi ambayo imechaguliwa kufanyika kwenye vijiji vyao, akisisitiza umuhimu wa kutunza nyaraka mbalimbali ili kuepukana na hoja za wakaguzi wa ndani na nje ya Halmashauri.
Diwani wa kata ya Mkwajuni Mhe. Shaibath Kapingu akizungumza katika kikao hicho, amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia Mkwajuni milioni 600, akisema kuwa kwa nguvu za wananchi wasingeweza kuwa na shule kama ambayo itajengwa kupitia fedha za Boost.
Mradi wa Boost unatekelezwa kwa miaka mitano ambapo utakelezaji wake unategemea na matokeo yatakayopatikana kwenye ujenzi wa mwaka wa kwanza.
Wilaya ya Songwe kupitia Mradi wa Boost imepokea bilioni 1,039,600,000 ambazo zinaenda kuboresha mazingira ya elimu awali na msingi.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.