Wakati masomo ya mhula wa kwanza kwa shule za sekondari na msingi nchini yakitegemewa kuanza Januari 09, 2023, wazazi wametakiwa kuwapeleka watoto shule kwa ajili ya kuanza kidato cha kwanza.
Wito huo umetolewa na Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Songwe Stephen Bange wakati akiongea ofisini kwake kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ambapo amesema umefika wakati wa wazazi kutambua umuhimu wa elimu, na kuachana na visingizio rahisi kama kukosa sare (uniform).
Bange amesema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kujenga na kuboresha mazingira ya elimu ikiwemo utoaji wa elimu bila malipo hivyo jamii inapaswa kuhamasika vya kutosha, akisema ifikapo Januari tisa mtoto yeyote anayepaswa kuwa darasani awe darasani bila kujalisha ana sare au hana.
"Kila mwanajamii anatakiwa kusisitiza mtoto aende shule, hakuna namna nyingine ya Songwe (Wilaya) kujikomboa kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa n.k bila kupata elimu. Hii ni elimu bila malipo, usipoipata sasa utaipata lini", alisema Bange
Afisa Elimu Sekondari huyo amesema Halmashauri ya Wilaya ya Songwe katika mwaka wa masomo 2023 inategemea kupokea wanafunzi 2,364 ambapo wanafunzi wote wataanza kusoma kwa pamoja kwani fedha zilizotengwa milioni 180 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan zimewezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa tisa na madawati wakati awali kulikuwa na mahitaji ya vyumba saba pekee.
Halmashauri ya Wilaya ya Songwe imekamilisha maandalizi ya kuwapokea wanafunzi hao kwani itakumbukwa Disemba 20, Mkurugenzi Mtendaji CPA Cecilia Kavishe alimkabidhi Kaimu Katibu Tawala Wilaya Chesko Mbilinyi vyumba vya madarasa tisa, Ofisi (Kanga Sekondari) na madawati vikiwa tayari kwa ajili ya kusomea watoto wa kidato cha kwanza wa mwaka 2023.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.