Mbunge wa Jimbo la Songwe Mhe. Philipo Mulugo amewafuta machozi watumishi wa Jeshi la Polisi katika Kituo kidogo cha Polisi cha Galula Wilayani Songwe kufuatia kutimiza ahadi ya kuwanunulia Pikipiki ambayo aliahidi kuwapatia Disemba 31, mwaka 2022.
Akikabidhi Pikipiki hiyo kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Songwe Maria Kway, Leo Jumatatu Machi 27, 2023, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Songwe Agapto Thomas Kilongozi amesema utoaji wa pikipiki hiyo ni sehemu tu ya mambo mengi ambayo yamekuwa yakitekelezwa na Mhe. Mulugo katika kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi.
Amesema mbunge mbali na kutoa pikipiki tayari amesaidia kufanya maboresho katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama.
"Mheshimiwa [Mulugo] yeye huwa anatoa huduma tu kwa Polisi kwa sababu anajua bila Polisi wananchi hawawezi kufanya shughuli za kiuchumi kwa amani", alisema Kilongozi ambaye ameeleza kuwa pikipiki hiyo imegharimu shilingi milioni 2,500,000 mpaka inafika Mkwajuni.
Maria Kway, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Songwe akizungumza baada ya kukabidhiwa pikipiki hiyo kama msimamizi mkuu wa Polisi Wilayani hapa amemshukuru Mhe. Mulugo kwa kutimiza ahadi waliyomuomba pamoja na kuendelea kutoa misaada mbalimbali kwa Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, Mrakibu Mwandamizi huyo amewaomba wadau wengine wa Polisi kuendelea kukishika mkono kituo hicho ili kifanane na hadhi ya Wilaya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Polisi Galula Petro Charles Masota ambaye atakuwa mlinzi wa kwanza wa pikipiki hiyo amesema usafiri huo utaenda kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Kipolisi Galula kwa wananchi.
Zoezi la ugawaji wa pikipiki hiyo uliofanyika Kituo cha Polisi Wilaya ya Songwe umehudhuriwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Saza, Galula na Mtendaji wa Kata ya Mkwajuni.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.