Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Songwe Ndg. Chesko Mbilinyi amewataka Maafisa Ugani waliokabidhiwa pikipiki 19, moja kwa kila mmoja kuhakikisha wanazitumia pikipiki hizo kwa matumizi ya ofisi, wakiwafikia wakulima, wafugaji wa hali ya chini wakiachana na tabia ya baadhi ya watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakitumia vyombo vya usafiri vya serikali kwenda kwenye maeneo ya starehe kama "Bar".
Kauli hiyo imetolewa Jumamosi nje ya Ofisi za Mkurugenzi Mtendaji zilizopo eneo la Kimborokoto wakati wa hafla ya kukabidhiwa pikipiki kwa Maafisa Ugani 19 ambazo zimeletwa ili kurahisisha utendaji kazi wa maafisa ugani hasa kwa Wilaya ya Songwe ambayo jiografia yake ni ngumu.
Ndg. Mbilinyi amewaeleza Maafisa Ugani kuwa waende wakazitumie pikipiki kama ambavyo serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekusudia.
"Wafikieni wakulima, wafikieni wafugaji zile changamoto za wafugaji kusema wanashindwa kufuga kwa sababu hawana elimu ziishe, wanufaika wa TASAF [Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini] wamekuwa wakisema hawana elimu ya ufugaji hakikisheni mnawafikia, mnawapa ushauri na elimu", alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe CPA. Cecilia Kavishe akizungumza katika hafla hiyo amewaambia Maafisa Ugani kuwa washirikiane na Watendaji wa Kata na Vijiji kusimamia ukusanyaji wa mapato.
Amesema itakuwa ajabu kama wamepewa pikipiki halafu mapato yataendelea kupotea, "tutakuwa hatutimizi lengo la Mheshimiwa Rais wetu".
CPA. Kavishe ametumia nafasi hiyo, kumpongeza Mheshimiwa Rais ambaye anaenda kutimiza miaka miwili madarakani kwa kuendelea kuwakumbuka watumishi na kuboresha mazingira ya utendaji wa kazi suala ambalo amelitaja kuwa linaongeza ari ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Andrew Kayombo, Afisa Kilimo na Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, akiongea kwenye zoezi hilo, amesema pikipiki ambazo zimepokelewa ni 19 na zimekabidhiwa kwa maafisa Ugani ambapo wale watakaoweza kuzitunza kwa muda wa miaka miwili, bodaboda hizo zitakuwa za kwao kama ambavyo maelezo ya wizara yanaeleza.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.