Mkuu wa Wilaya ya Songwe mkoani Songwe Mhe. Simon Simalenga amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe kuwa na utamaduni wa kuwasiliana na kujuliana hali ili kudumisha upendo miongoni mwa watumishi hao kwa kuunda makundi "groups" za Whatsaap katika kutengeneza udugu kati yao.
Mhe. Simon Simalenga ametoa mwito huo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Songwe ukiwa ni utaratibu wa kawaida wa kuwa na vikao vya kila baada ya muda, ambapo ameeleza kuwa kutokana na utafiti alioufanya amebaini kuwa kumekuwa na uhafifu wa mawasiliano kati ya mtumishi na mtumishi, watumishi wa makao makuu na watumishi waliopo nje ya makao makuu (HQ) suala linalopelekea utoaji wa huduma kuwa hafifu pia.
Mhe. Simalenga amehusisha uhafifu wa mawasiliano na uhafifu katika utoaji wa huduma kwa wananchi ambapo ameelekeza kuwa kwa sasa makundi yaundwe kuanzia idara husika na kundi la watumishi kwa ujumla ili kuwasiliana na kupeana faraja wakati wa dhiki.
"Kila mmoja anapambana na matatizo yake, hata likimshinda hana sehemu ya kuuliza, hiyo haiwezekani". Alisema Mhe. Simalenga wakati kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Sambila.
Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa endapo kutakuwa na mawasiliano na mahusiano ya karibu ambayo kwa wakati huu wa teknolojia huletwa na mitandao ya kijamii ikiwemo Whatsaap utolewaji wa huduma kwa wananchi utaimarika, watumishi watashirikiana katika kutatua matatizo na changamoto za wananchi ambapo pia kutakuwa na umoja miongoni mwa watumishi wa makao makuu, wakuu wa idara na wale wa nje ya Halmashauri.
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Songwe kutoka idara ya Elimu Msingi na Sekondari, Kilimo na Madereva wakizungumza kwenye kikao hicho wamesema tayari wameanza kutekeleza kwa vitendo agizo la Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kwa kuunda makundi ya Whatsaap ambayo sasa yanawaunganisha pamoja.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.