Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Songwe Chesko Mbilinyi amewataka wazazi ambao watoto wao wamefaulu kujiunga na kidato cha kwanza 2023 kuhakikisha wanafanya hivyo kuanzia Januari Mosi 09.
Kaimu Katibu Tawala Chesko Mbilinyi ametoa wito huo wakati akikabidhiwa vyumba vya madarasa 9 vikiwa na madawati ndani kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ambavyo vimejengwa na kukamilika vikiwasubili wanafunzi wa kidato cha kwanza 2023, tukio lililofanyika katika Shule ya Sekondari Kanga (vyumba vitatu na Ofisi), Sume na Namalaji.
Ndg. Mbilinyi amesema haitakuwa na maana kama vyumba vya madarasa vimekamilika lakini vikakosa wanafunzi kwa makusudi ya mzazi au mlezi.
“Ndugu zangu wazazi madarasa haya ni ya kwenu, watoto wenu wanatakiwa kusoma kwenye hayo madarasa, msiwafiche vijana wenu”. Alisema.
Pia, Kaimu Katibu Tawala huyo amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe pamoja na wataalamu kwa kusimamia vizuri ujenzi vya vyumba vya madarasa, ofisi na madawati, akisema usimamiaji huo ndiyo dhana ya uzalendo na uwajibikaji.
CPA Cecilia Kavishe, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe akizungumza baada ya kukabidhi vyumba vya madarasa na madawati vilivyokamilika kwa asilimia 100 kwa Kaimu Katibu Tawala ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha milioni 180 kwa ajiili ya ujenzi wa madarasa tisa, madawati na ofisi katika shule ya sekondari Kanga.
“Leo (Disemba 20, 2022) ni siku ya kipekee kwani tunakabidhi madarasa, madawati na ofisi vikiwa vimekamilika. Tunampongeza sana Mhe. Rais kwa kutuletea fedha hizi wananchi wa Songwe, wanafunzi 450 siyo wachache wanaotarajia kuanza kuyatumia madarasa hayo”. CPA Cecilia alitoa pongezi hizo akiwa katika Shule ya Sekondari Kanga.
Mwakilishi wa wananchi kata ya Kanga Mhe. Erick Kihinda amesema ujenzi wa vyumba vya madarasa vitatu na ofisi katika kata yake itaenda kuongeza imani ya wananchi kwa viongozi wao, wataona serikali imethamini kwani watoto wao hawatasoma kwa shida tena.
Jumla ya wanafunzi 2,364 wanategemea kuanza masomo ya kidato cha kwanza wilayani Songwe kwa mwaka 2023 ambapo kati ya wanafunzi hao, 450 ikiwa na maana ya wanafunzi 50 kwa kila darasa watatumia madarasa hayo mapya ambayo yamejengwa kwa fedha maarufu kama “Pochi la Mama”.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.