Wanufaika vijana wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Songwe wametakiwa kuchukua tahadhari katika namna ya kuendesha pikipiki ambazo wamekabidhiwa ili waepukane na ajali ambazo zinazaweza kujitokeza kutokana na uzembe wa kutokuwa makini barabarani.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe Mhe. Abraham Kaguluka Sambila wakati akikabidhi pikipiki 47 kwa vikundi 9 vya vijana zenye thamani ya shilingi milioni 123,140,000 kutokana na mapato ya ndani, shughuli iliyofanyika nje ya Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji iliyopo Kimborokoto, Mkwajuni Aprili 06, 2023.
Mhe. Sambila amesema pamoja na lengo la serikali la kuwanufaisha vijana kiuchumi lakini mikopo itakosa maana kama vijana ambao wamekopeshwa hiyo mikopo wataishia kuwa wenye ulemavu kutokana na madhara ya kutotumia vizuri pikipiki kwa kuzingatia taratibu za barabarani.
“Lakini kubwa kuliko ni usalama wenu, pikipiki hizi zitakosa maana kama mtaishia kuwa walemavu. Vijana wangu, pikipiki zinaua, mkishindwa kuwa waangalifu wa kufuata sheria za barabarani mtakuwa walemavu na sisi Halmashauri tutakuja kukudai tu na ulemavu wako, kwa hiyo nendeni mkawe waangalifu”, alisema Mhe. Sambila ambaye ni Diwani wa Kata ya Mbangala.
Diwani huyo pia amewaeleza vijana kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Songwe itaendelea kukopesha mikopo kwa makundi yote kama ambavyo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiagiza lengo likiwa ni kuwapa ajira na kuwapa uchumi mzuri wananchi wake kupitia mikopo hiyo isiyokuwa na riba.
“Tutaendelea kutoa mikopo kama ambavyo tunaelekezwa. Lengo mpate ajira maana siyo lazima uje hapa ofisini ndiyo ujione kama umeajiriwa, pikipiki ni ajira kama zilivyo ajira nyingine”, aliongeza.
Abdallah Mgonja, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe amewahimiza vijana kuwekeza nguvu kubwa katika marejesho ili waweze kumaliza mapema wabakie na umiliki kamili wa pikipiki angalia zikiwa mpya.
“Tunategemea nyinyi baada ya hapa mtaanza kazi rasmi na mapato yenu kipaumbele cha kwanza inatakiwa mfikirie kufanya marejesho, bora mjinyime saizi mfanye marejesho haraka ili muwe huru na pikipiki zenu wenyewe”, alisema Mgonja, Mtaalamu wa Misitu na Maliasili.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mikopo ya Halmashauri ya wilaya ya songwe, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Thomas Kiwoi amesema kwa mwaka wa fedha 2022-2023, Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ilipanga kukopesha shilingi milioni 304,480,000 ambapo katika robo ya tatu [Januari–Machi] Halmashauri ya Wilaya ya Songwe imeshakopesha jumla ya shilingi milioni 175,74,500 na kwa kundi la vijana wamekabidhiwa vijana pikipiki 47 shilingi milioni 123,140,000.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.