Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe CPA Cecilia Kavishe amewataka watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa mapato kutumia njia shirikishi wakati wa ukusanyaji kuliko kutumia mabavu ambayo amesema hayatakuwa na matokeo endelevu.
CPA Cecilia Kavishe ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kikao na Wenyeviti wa waendesha Bajaji, Bodaboda na Mwenyekiti wa Wafanyabishara wa Stendi Mpya Kata ya Mkwajuni na Wilaya ya Songwe ambapo amesema Bodaboda na waendesha bajaji wakipewa elimu kuhusu umuhimu wa ushuru watatoa bila usumbufu.
Amesema lazima washirikishwe, wajue kinachoendelea na kitawaletea faida zipi wao wenyewe na serikali kwa ujumla ambapo ametolea mfano wa mapato ya vibanda vya sokoni ambavyo vilikuwa na shida kubwa katika ukusanyaji lakini saizi Halmashauri imekuwa ikikusanya baada ya kuwashirikisha.
"Muda mwingine tunapata changamoto kwenye kukusanya ushuru kwa sababu hatujawaelimisha. Wapeni elimu, washirikishine ili walipe na waone matokeo yake", alisema CPA Cecilia Kavishe wakati wa kikao hicho kilichofanyika Ofisini kwake Leo Jumatatu Machi 20, 2023.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji huyo amewasihi waendesha bajaji na pikipiki kwa jinsia zote kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 ambayo imekuwa ikitolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Songwe kupitia mapato ya ndani.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mwenyekiti wa Bajaji Kata ya Mkwajuni Noah Shitente, Mwenyekiti wa Bodaboda Godfrey Fredrick na Yusta Abel Mwakilishi wa uongozi wa Wafanyabishara wa Stendi Mpya ya Wilaya ambao wameishukuru Halmashauri kwa kuwashirikisha katika mipango yao pamoja na kuomba wawe wanapewa taarifa mapema za mabadiliko ya ushuru na kodi mbalimbali.