Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe amewasihi wakulima wa kilimo cha ufuta Wilayani Songwe wajiunge na vyama vya ushirika ambavyo vitawasaidia kuwa na kilimo chenye tija na manufaa kwao na Halmashauri.
Mhe. Wangala amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea kata za Bondeni, Tarafa ya Songwe kutoa elimu na kuhamasisha wakulima wa ufuta kujiunga na vyama vya ushirika ambavyo utawafanya kuwa pamoja na stakabadhi ghalani ndiyo itakuwa suluhisho la upatikanaji wa bei nzuri, pembejeo za kilimo, ushauri wa kitaalamu sambamba na kupata mikopo yenye riba nzuri.
Akiwa ameambatana na Watalaamu wa kilimo na ushirika kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Mhe. Wangala ameongeza kuwa mateso ambayo wakulima walikuwa wanapata wataachana nayo kwa kujiunga na ushirika na stakabadhi ghalani.
"Serikali imeona (wakulima) tunaonewa, bei zinakuwa mbaya, mikopo wanatupa haina afya kwenye ustawi wetu, sasa wametuletea stakabadhi ghalani, tujiunge wakulima wenzangu", alisema Mheshimiwa Wangala akizungumza kata ya Mpona.
"Niwaambie sisi tumeenda kujifunza kwa wenzetu wa Lindi wanavyofanya, tumeona mfumo huu (stakabadhi ghalani) ni mkombozi wetu kwa sababu bei ya ufuta wetu itakuwa na ushindani lakini pia tutakuwa na bima endapo majanga yatatokea", alisema Mhe. Wangala akimuwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songwe Mhe. Abrahamu Sambila.
Diwani wa kata ya Manda Mhe. Joseph Maige Machumu ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira akizungumza na wananchi wa Kata ya Mpona na Totowe amewasihi wananchi hao kutumia vizuri uhuru wa kujiunga na vyama vya ushirika kwa kuamua kujiunga navyo kwani wakulima watakao kuwa wamejiunga wataweza kuhifadhiwa ufuta wao na kuwauzia bei nzuri ambayo wanunuzi wameshindana tayari.
Mhe. Maige amewasihi wakulima ambao watakuwa tayari kuingia kwenye vyama vya ushirika kuhakikisha wanachagua viongozi imara ambao watakuwa na uwezo wa kusimamia mahitaji ya wakulima.
Afisa Ushirika wa Halmashauri David Mbembela akiongea wakati wa kutoa hamasa hiyo amesema vikundi vya ushirika vinatakiwa kuwa na watu angalau 30 au kuendelee ambapo kwenye vikundi hivyo kutakuwa na viongozi ambao watawaongoza wengine.
Kaimu Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya Andrew Kayombo amesema pamoja na kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani utarahisisha ukusanyaji wa mapato kwa Halmashauri lakini pia mfumo huo utawapa wataalamu wa kilimo urahisi wa kwenda kutoa elimu ya kilimo.
Ziara ya kutoa elimu kwa wakulima wa ufuta kwa kata za bondeni awamu ya kwanza imeshafika kata ya Totowe, Namkukwe, Mpona na Manda.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.