Wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Akiba Kata ya Udinde Wilayani Songwe mkoani Songwe wametakiwa kutumia mafunzo waliyopata ya kizalendo kutunza amani na utulivu ya wananchi wa Songwe na taifa kwa ujumla.
Wahitimu hao 85, wakiume 62 na wanawake 23 wamepewa agizo hilo na Mkuu wa Wilaya ya Songwe ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo Mhe. Simon Simalenga amesema hayo wakati akifunga mafunzo yaliyofanyika kwa miezi minne katika Kata ya Udinde.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe. Simalenga amesema mafunzo waliyopata wahitimu hao kuwa chachu katika kujua namna ya kuilinda na kuitetea nchi.
Amesema itakuwa ajabu kama watu waliopata mafunzo wanajihusisha na uhalifu badala ya kutunza amani, kuchochea ugomvi badala ya kuwa sehemu ya kimbilio kutokana na uzalendo mliofundishwa.
"Aaah sitaki kusikia habari za uhalifu hapa, nataka muwe chanzo cha amani" alisisitiza Mkuu wa Wilaya.
Pia, wahitimu wametakiwa kutumia elimu waliyoipata katika kujiingiza katika shughuli za kuzalisha ili waweze kuwa na kipato chao wenyewe.
Chesko Mbilinyi, Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Songwe amewahimiza wahitimu wa mafunzo hayo kushiriki katika kampeni ya kuzuia uvuaji haramu wa samaki Ziwa Rukwa, "najua wengi wanaovua kwa kutumia nyavu zisizo rafiki kama kokoro na timba siyo wenyeji wa hapa (Udinde), wakomesheni hao".
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe CPA Cecilia Kavishe akizungumza katika siku ya hitimisho la mafunzo ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza katika kata ya Udinde tangia mwaka 1999 amesema atawaelekeza wataalamu wa maendeleo ya jamii wa Halmashauri kutenga muda kuja kuwafundisha juu ya mikopo ya 10% ili wale watakaokuwa na uhitaji na sifa wapatiwe mikopo kwenye kundi la vijana.
Mafunzo hayo hufanyika kila mwaka ambapo Frank Cibaya, Mkuu wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Songwe akisoma taarifa ya mafunzo hayo alisema kuwa wanafunzi walianza 216; 25 (23) katika idadi hiyo walikuwa ni wanawake.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.