Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe CPA Cecilia Kavishe ameitumia Siku ya Kumbukizi ya Kuzaliwa kwake (Octoba 29) kwa kushiriki chakula cha mchana na kukata keki pamoja na Wanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kapalala ambayo iko Tarafa ya Kwimba.
Mkurugenzi Mtendaji CPA Cecilia ameshiriki tukio hilo Leo Jumamosi Novemba 13, 2021 ambapo ametumia wasaa huo kuwahamasisha Wanafunzi wafanye vizuri na waondoa hofu wakati wote watakaokuwa kwenye vyumba vya mitihani hali kadhalika katika maandalizi ya mwisho.
Amesema hakuna mbadala wa elimu, hakuna haja ya kuwa na hofu, akiwataka kila mmoja kutambua kuwa miaka minne ambayo wamekaa shuleni siyo hivyo wajitahidi kufanya vizuri kwenye mitihani wa mwisho ambayo utakuwa urithi wao wenyewe na fahari kwa wazazi na walezi.
Aidha, CPA Cecilia amewashukuru Wazazi/Walezi kwa kuwasimamia watoto wao kuhakikisha wanahitimu masomo mbali na changamoto kwa baadhi ya wanajamii kukosa mwamko wa elimu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Kapalala Raimos Benson Mwashilindi akizungumza kwa niaba ya Waalimu na wazazi amempongeza Mkurugenzi Mtendaji CPA Cecilia, akisema zawadi aliyoitoa kwao ya kushiriki sherehe ya kuzaliwa na Wanafunzi ni tukio kubwa na la kipekee hasa ikiwa Shule hiyo haikufanya mahafali.
"Mama tunakupongeza, maana una Shule nyingi Wilayani hapa, ungeamua kwenda kula keki sehemu nyingine lakini umekuja hapa, Mungu akubariki", alisema Mwashilindi katika sherehe hiyo fupi iliyofanyika katika moja ya darasa shuleni hapo.
Naye, Rose Mwakalindile, Kaimu Afisa Elimu Sekondari ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji ambapo pia amewasihi Wanafunzi kuendelea kujisomea mpaka siku ya mwisho akisema kwenye elimu Ng'ombe hunenepa siku ya mnada tofauti na usemi wa wahenga.
CPA Cecilia Kavishe aliamua kula chakula cha mchana na kukata keki pamoja na Wanafunzi hao ikiwa ni sehemu ya kutakia kheri.
Jumla ya wanafunzi 28 wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kapalala wanategemea kuanza mitihani ya kuhitimu masomo yao siku ya Jumatatu Novemba 15, ambapo Wanafunzi wa kike ni watatu (3) pekee.
Mkwajuni-Kimborokoto - Saza Road
Anuani ya Posta: P.o.Box 77 Mkwajuni Songwe
Mawasiliano: +255 (025) 2520301
Simu: +255 (025) 2520301
Barua Pepe: ded@songwedc.go.tz
Copyright ©2020 Songwe District Council . All rights reserved.